Mwili wa mchimba dhahabu wapatikana baada ya miezi 8

 Mwili wa mchimba dhahabu Tom Okwach ulipatikana Jumapili, baada ya siku 205, tangu timbo la Abimbo, Kaunti ya Siaya, kuporomoka Desemba 2, 2021.

Wakazi walikuwa wakichimba mtaro karibu na timbo hilo walipoupata mwili huo.

Bw Okwach alikuwa kati ya wanaume wanane waliozikwa na mchanga baada ya timbo hilo kuporomoka. Hata hivyo, wachimbaji sita walinusurika mkasa huo, huku wawili kati yao wakiaga dunia. Mwili wa Enos Ong’ong’a uliopolewa kwenye timbo hilo mnamo Desemba 5.

Karibu wachimbaji 15 walikuwa wamejitolea kuendelea kuutafuta mwili huo, baada ya wazima-moto na vikosi vya kukabiliana na mikasa kutoka serikali ya Kaunti ya Siaya kukata tamaa.

Mmoja wa manusura alisema alikuwa amesikia mtikisiko wa ardhi akiwa ndani ya timbo hilo, ijapokuwa kauli yake ilipuuzwa na msimamizi wao.

Okwach alimwacha mjane na watoto wawili.

Mjombake marehemu, Bw Fred Ogude, aliiambia ‘Taifa Leo’ kwamba tayari washaanza mipango ya mazishi, baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kujua hatima ya jamaa yao.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii