Tetemeko la ardhi mashariki mwa Afghanistan lauwa karibu watu 920

Tetemeko kubwa la ardhi limetikisa mashariki mwa Afghanstan mapema leo na kusababisha vifo vya karibu watu 920. Maafisa wamesema mamia ya watu wamejeruhiwa na na kuwa idadi ya vifo inatarajiwa kupanda wakati waokozi wakiendelea na shughuli ya kupekua kwenye vifusi. Tetemeko hilo la ardhi lililouathiri kabisa mkoa wa Paktika limetokea katika wakati ambao jamii ya kimataifa kwa kiasi kikubwa imeondoka Afghanistan baada ya Taliban kuchukua madaraka mwaka jana kufuatia kuondoka kwa jeshi la Marekani nchini humo. Hali hiyo itafanya juhudi zozote za uokozi na msaada kuwa ngumu katika nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 38. Kiongozi wa juu wa Afghanistan Hibatullah Akhundzada amesema idadi ya vifo imepanda wakati taarifa zikiendelea kumiminika kutoka maeneo ya milima ambayo sio rahisi kufika.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii