Mamia waandamana kupinga mabadiliko ya katiba Tunisia

Mamia ya watu wameandamana Jumapili katika mji mkuu wa Tunisia wakipinga mpango wa kura ya maoni kubadili katiba na hatua ya hivi karibuni ya Rais Kais Saied ya kuwafukuza kazi darzeni ya majaji.

Waandamanaji mjini Tunis wameitikia wito wa makundi ya upinzani, ikiwemo chama hasimu cha Saied cha kiislamu cha Ennahdha, wakiimba "katiba, uhuru, na utu", na "wananchi wanataka mahakama huru", mwandishi wa habari wa AFP amesema.

Katiba mpya ni sehemu ya mipango ya mageuzi ya Saied na itarajiwa kupelekwa kwenye kura ya maoni tarehe 25 Julai, mwaka mmoja baada ya kuifuta kazi serikali na kulisimamisha bunge.

Tangu wakati huo alijiongezea mamlaka, ikiwemo kulivunja bunge mwezi Machi.

Mapema mwezi huu, aliwafuta kazi majaji 57, baada ya kuwashtumu wengi kula rushwa na uhalifu mwingine.

"Kura ya maoni sio kitu kingine isipokuwa udanganyifu,", amesema Ali Layaredh, kiongozi kutoka chama cha Ennahdha, ambacho kilikuwa chama kikuu katika bunge na katika serikali iliyofutwa kazi na rais.

"Tunaandamana dhidi ya kuitenga mamlaka ya mahakama na dhidi ya mapinduzi ambayo yanailenga katiba," amesema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii