Ujerumani na Marekani kutuma silaha za kisasa Ukraine

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema nchi yake itapeleka Ukraine makombora ya kisasa ya kuzuia mashambulizi ya kutokea angani pamoja na mifumo ya radar. Hii ni baada ya Ujerumani kukosolewa kwa kutochukua hatua za kuisaidia Ukraine kuikabili Urusi. Uamuzi wa Ujerumani umekuja baada ya Rais Joe Biden kusema Marekani itapeleka mifumo ya kisasa ya makombora ya wastani nchini Ukraine. Mifumo hiyo ya makombora ni sehemu ya kitita kipya cha dola milioni 700 cha msaada wa masuala ya usalama kwa Ukraine kutoka Marekani unaojumuisha helikopta, mifumo ya silaha za kuzuia mashambulizi ya vifaru, magari ya kijeshi na mambo mengine. Uamuzi huo wa Marekani kutoa zana za kisasa za makombora unajaribu kuweka mizani kati ya nia ya kuisaidia Ukraine kupambana dhidi ya mashambulizi makali ya Urusi na wakati huo kutoipa Ukraine silaha ambazo zitaiwezesha Ukraine kuyapiga maeneo ya ndani ya Urusi na kuchochea kuongezeka kwa vita hivyo. Viongozi wa Ukraine wamekuwa wakiomba kupewa zana hizo za kisasa wakati wakipambana kuzuia harakati za Urusi katika mkoa wa mashariki wa Donbas.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii