KIJANA AFARIKI AKIWA KWENYE CLUB.

MCHUANO wa fainali za kombe la mabingwa wa UEFA, uligeuka kuwa simanzi kwa familia moja Kaunti ya Kilifi.

Hii ni baada ya jamaa wao kuuawa kilabuni alikoenda kutazama mechi hiyo kati ya Liverpool na Real Madrid usiku wa kuamkia Jumapili.

Polisi katika Kaunti ya Kilifi wamewatia mbaroni washukiwa wawili kufuatia kifo cha mwanamume huyo kilichotokea katika Lexo Lounge, mwendo wa saa saba usiku.

Familia ya Feisal Bushiti Mukongo, 30, iliambia Jembe FM alikuwa ametoka katika mazishi ya jirani wao alipoamua kwenda kutazama fainali ya UEFA.

Duru zilisema, mvutano ulitokea baina yake na walinzi wa kilabu mlangoni.

“Alikuwa amelipa kiingilio lakini aliyekuwa akichukua pesa hizo mlangoni alikuwa hataki kumrudishia chenji. Walianza kuzozana ndipo mtunza fedha aliwaita walinzi ambao bila kutaka kujua yaliyojiri, walimvamia na kuanza kumpiga hadi wakamuua,” akasema mjombake, Bw David Mwanzele.

Bw Mwanzele alisema kuwa madaktari walithibitisha mwathiriwa alikuwa amefariki alipofikishwa Hospitali Kuu ya Rufaa ya Kilifi.

“Tunashuku alipata majeraha ya ndani ya mwili kwa sababu hakuwa na majeraha yoyote yaliyoonekana kwa mwili,” amesema.

Vijana walizua vurugu na kuchoma tairi huku wakifunga barabara kuu ya Kilifi-Mombasa usiku kufuatia kisa hicho.Iliwalazimu polisi kufyatua risasi hewani na kutumia vitoa mchozi kuwatawanya vijana.

Bi Anne Kuto, dadake marehemu, ameitaka serikali ya kitaifa na ile ya kaunti kuhakikisha kuwa wanapata haki.Alisema marehemu alikuwa tegemeo kwa familia yake kupitia kwa vibarua alivyofanya na kwamba amemwacha mjane na watoto wachanga wenye miaka minne na miwili.

“Mke wake sasa amebaki mpweke bila matumaini,” amesema.

Alithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Kilifi Kaskazini, Bw Jonathan Koech, alisema kuwa washukiwa waliokamatwa ni meneja wa kilabu hiyo na mmoja wa walinzi.Alisema wamezuiliwa ili kuwasaidia polisi katika uchunguzi wa kifo hicho.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii