Rais wa Marekani Joe Biden ametembelea familia za wanafunzi 19 na walimu wawili, waliouawa kwa kupigwa risasi wakiwa shuleni wiki iliyopita katika mji wa Uvalde, jimboni Texas.
Biden na mkewe walibubujikwa machozi walipofika eneo la kumbukumbu ya wahanga ambako kuna picha za wanafunzi na walimu waliouwawa pamoja rundo la mashada ya maua na kadi zenye salamu nyingi za rambirambi kutoka kwa watu walioguswa na mkasa huo.
Wakiwa wamevalia mavazi meusi yanayoashiria maombolezo, rais Biden na mkewe walitembea taratibu kutazama picha ya kila aliyepoteza maisha wakati wa shambulizi la wiki iliyopita ambalo linatajwa kuwa baya zaidi kuwahi kutokea nchini Marekani kwa karibu muongo mmoja.
Naye Makamu wa rais Kamala Harris, amesema wakati umefika wa kusitsiha matumizi mabaya ya bunduki nchini humo.
Wakati huo huo, idara ya haki imesema itachunguza namna polisi walivyoshughulikia tukio hilo ambalo limezua hasira nchini Marekani, kuhusu kuendelea kwa matukio ya watu kupigwa risasi mara kwa mara.