Majeshi ya Urusi yaishambulia miji ya mashariki mwa Ukraine

Vikosi vya Urusi vimeongeza kasi ya mashambulizi dhidi ya mji wa Sievierodonetsk mashariki mwa Ukraine baada ya kudai kuutia mkononi mji wa Lyman. Lengo kuu ni kuvizingira vikosi vya Ukraine.

Kwa mujibu wa taarifa wanajeshi wa Urusi wanakaribia kuliteka eneo lote la Luhansk katika jimbo la Donbas, kwenye vita, ambavyo sasa vimeingia katika mwezi wake wa nne tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

Polisi walichapisha kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumamosi kwamba mji wa Sievierodonetsk umekabiliwa na mashambulio makali ya vikosi vya Urusi.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa eneo la Lysychansk-Bakhmut pia limekabiliwa na mashambulizi makali ambapo majeshi ya Urusi yanalenga kuuchukua ili kuweza kuvizingira vikosi vya Ukraine. Polisi ya Ukraine imesema kumetokea uharibifu mkubwa katika mji huo wa Lysychansk.

Mshauri wa rais wa Ukraine ambaye pia anaiwakilisha nchi yake kwenye mazungumzo ya amani, Mykhailo Podolyak ametoa wito huo kwa nchi yake kupewa magari ya kijeshi yanayoweza kurusha makombora mengi ya masafa marefu kwa wakati mmoja kutoka Marekani. Maafisa wa Marekani wameliambia shirika la Habari la Reuters kwamba ombi la Ukraine linazingatiwa na uamuzi utatolewa katika siku zijazo.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameonyesha matumaini katika hotuba yake kwa njia ya video kwamba washirika wataipa nchi yake silaha zinazohitajika kufikia wiki ijayo.

Zelenskiy amesema haamini wazo la kutumia nguvu ili kuikomboa ardhi yote Ukraine iliyonyakuliwa na Urusi tangu mwaka 2014, ambayo pia inajumuisha jimbo la Crimea.

Katika juhudi za kidiplomasia kuwezesha kupatikana suluhu kwenye vita vya Ukraine rais wa Ufaranya Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz walizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Jumamosi ambapo walimuhimiza juu ya kuondoa vizuizi kwenye bandari ya Odesa na kuruhusu usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine.

Viongozi hao wamesema rais wa Urusi Vladmir Putin aliwaambia kwamba nchi yake iko tayari kujadili njia zizakazoiwezesha Ukraine kuanza tena usafirishaji wa nafaka kutoka kwenye bandari zake katika Bahari Nyeusi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii