Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Guaido ashambuliwa

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela aliyejitangaza kuwa rais wa mpito Juan Guaido, ameshambuliwa kimwili hapo jana.Video zilizochapishwa katika mitandao ya kijamii na tovuti ya kituo cha habari cha El Nacional zilionesha Guaido akitukanwa, kusukumwa na kurushiwa vitu wakati wa ziara yake katika jiji la San Carlos jimboni Cojedes. Picha moja ilimuonesha Guaido na shati lililochanika ijapokuwa haikubainishwa awali ikiwa alijeruhiwa. Katika taarifa, ofisi ya Guaido imesema kuwa washambuliaji waliokuwa wamejihami kutoka kwa kambi iliyoiita ya kidikteta ya rais Nicolas Maduro walimshambulia vibaya kiongozi huyo na kuwapiga wafuasi wake. Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba gari alilotorokea Guaido lililengwa kwa risasi kadhaa. Katika ujumbe kupitia mtandao wa twitter, Brian Nichols kutoka timu ya masuala ya rasi ya Magharibi katika ofisi ya mambo ya nje ya Marekani, amesema wamesikitishwa na shambulio hilo dhidi ya rais Guaido na wafuasi wake na kwamba lilitishia maisha.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii