Ukraine yasema imeyapiga maeneo ya wanajeshi wa Urusi mkoani Kherson

Ukraine imesema leo kuwa imeyapiga maeneo ya jeshi la Urusi katika mkoa wa kusini wa Kherson ambako jeshi la Kyiv linapambana kulikomboa eneo lililokamatwa na wanajeshi wa Moscow katika siku za mwanzo za uvimizi. Wizara ya ulinzi imesema ndege za kivita za Ukraine zimefanya mashambulizi ya kutokea angani na katika maeneo ambako kuna zana za kivita na askari pamoja na maghala katika maeneo matano tofauti ya mkoa wa Kherson. Katika upande wa mashariki, Ukraine imesema vikosi vyake vinakabiliwa na mashambulizi makali ya Urusi, wakati vikijitahidi kushikilia ngome zao katika maeneo muhimu ya mji wa Severodonetsk. Ikiwa Urusi itaukamata mji huo itaweza kuudhibiti ukanda wa Donbas, na pia mto muhimu wa Donets. Ukanda huo una viwanda vingi, na kuumiliki kutaisaidia Urusi kuweka kiunganishi cha nchi kavu na rasi ya Crimea iliyoinyakuwa kutoka kwa Ukraine mwaka 2014.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii