MTU na mkewe waliokuwa wametengana kwa miezi mitatu walifariki saa chache baada ya kurudiana pikipiki walimosafiria ilipogongana na lori kwenye msafara wa kampeni kaunti ya Meru.
Jackson Mawira alikuwa akirudi nyumbani na mkewe Nancy Kendi miezi mitatu baada ya kutengana ajali hiyo ilipotokea karibu na soko la Keria katikati ya miji ya Nkubu na Chogoria.
Mawira, mwanabodaboda mwenye umri wa miaka 28 alifariki katika eneo la ajali huku mkewe aliyepata majeraha mabaya akifariki katika hospitali ya St Anne alikokimbizwa.
Mtoto wao mwenye umri wa mwaka mmoja alijeruhiwa kwenye ajali hiyo na anaishi na dada ya baba yake Bi Irene Nkatha.
Bi Nkatha alisema kwamba kabla ya ajali, ndugu yake alikuwa na furaha ya kurudiana na mkewe.
Furaha yake ilikatizwa wakati pikipiki aliyokuwa akiendesha ilipogongana na lori lililokuwa likibeba wafuasi wa mgombeaji wa kiti cha eneobunge la Imenti Kusini Dkt Shadrack Mwiti wa chama cha Jubilee.
“Tulihuzunika sana tulipopokea habari za tanzia lakini sasa tumekubali mapenzi ya Mungu. Hata kama walikuwa wametengana kwa muda, tunajua kwamba roho zao ziko pamoja kwa kuwa walikuwa wameridhiana,” akasema Bi Nkatha, na kuongeza kuwa wanandoa hao watazikwa Alhamisi .
Hata hivyo, alisikitika kuwa wameachiwa mzigo wa kulipa bili ya hospitali licha ya mwanasiasa huyo kuahidi kuwasaidia.
“Kufikia sasa tumechangisha zaidi ya Sh40,000 za upasuaji wa mwili na ada za mochari. Lakini hatujui tutakapopata pesa za kugharimia mazishi na kutunza mtoto aliyeachwa yatima,” alisema.
Jana, msaidizi wa mwanasiasa huyo Bw Mwenda Nchamba alikiri kwamba alikuwa amejitolea kulipa baadhi ya bili bila kufafanua zaidi.
Kisa hicho kinafuatia kingine ambacho gari la mbunge wa Borabu Kaunti ya Nyamira liligonga watu alipokuwa akuhutubia mkutano wa kampeni mwishoni mwa wiki jana.
Mbunge huyo alishutumiwa vikali kwa kupuuza kisa hicho na kuendelea kuhutubia watu akiwaomba kura bila kushtuka.
“Ni kweli kwamba mojawapo ya magari katika msafara wangu, aina ya Toyota Land Cruiser lilihusika katika ajali katika soko la Nyaramba, Borabu tukielekea Kebirigo. Breki za gari hilo zilifeli na kusababisha kisa hicho cha kusikitkisha,” alisema.
Kwenye video iliyosambazwa mtandaoni, Bw Momanyi anaonekana kutoshuka gari hilo lilipopita kwenye umati na kujeruhi mtu mmoja huku akiwataka wakazi kuendelea kusikiliza hotuba yake.
Licha ya watu kusikika wakipiga kelele kumweleza gari lilikuwa limeingia kwenye umati na mtu mmoja alikuwa amepata majeraha, Bw Momanyi anaonekana kutojali.
Watu wengi walikasirishwa na tabia ya mwanasiasa huyo ya kupuuza ajali mbaya ambayo ingeua watu huku wengine wakimlaumu kwa kukosa utu.