Mvutano wa kidiplomasia kati ya China na Canada unaongezeka tena, wakati kila mmoja akimshtumu mwenzake kwa uchochezi kwa kutumia ndege zao za kijeshi zinazoruka karibu na Korea Kaskazini. Mapema Jumatatu, wizara ya mambo ya nje ya China iliionya Canada kwamba huenda ikakumbana na matokeo mabaya iwapo itaendelea na uchochezi wa aina yoyote ile, baada ya jeshi la Canada wiki iliyopita kuishtumu China kwa kutuma ndege zake za kivita kuzihangaisha ndege za Canada zilizokuwa zikishika doria katika anga ya Korea Kaskazini. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Zhao Lijian amewaambia wanahabari kuwa, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa halijawahi kuiidhinisha nchi yoyote kufanya doria za kijeshi katika bahari au anga ya nchi nyengine kwa kisingizio cha kutekeleza vikwazo. Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau alijibu kwa kusema ndege za Canada zilikuwa zinashiriki katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa.