Msako wa kuwatafuta waliofanya shambulizi kanisani Nigeria unaendelea

Mamlaka na mashahidi wamesema shambulio katika kanisa katoliki magharibi mwa Nigeria limeonyesha kila dalili kwamba lilikuwa ni tukio la kupangwa. Licha ya washambuliaji hao kutotambulika, wataalamu wanasema washambuliaji hao wanatokea sehemu nyengine ya taifa hilo la Afrika Magharibi ambalo linakumbwa na ghasia kutoka makundi ya silaha, watekaji nyara na wapiganaji wenye itikadi kali. Eric Humphery-Smith, mtaalamu katika kampuni ya kijasusi ya Verisk Maplecroft ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, shambulio hilo ni la kigaidi na kutokana na idadi ya wahanga na kwa namna walivyouawa, inaonyesha lilipangwa kwa uangalifu mkubwa na wala sio shambulio la kushtukiza. Kamishna wa polisi wa jimbo hilo Oyeyemi Oyediran amesema vikosi vya usalama likiwemo jeshi liliwaandama washambuliaji hao lakini kwa bahati mbaya, hawakufanikiwa kuwakamata. Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na mauaji hayo ya kinyama. Mbunge mmoja katika jimbo la Ondo amesema takriban watu 50 walipoteza maisha yao katika shambulio hilo huku makumi ya wengine wakijeruhiwa, japo idadi kamili ya wahanga haikutolewa na wafanyikazi wa hospitali katika jimbo hilo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii