Mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podoliak amesema mbinu za Urusi zimebadilika katika vita nchini humo na kuashiria kile alichokiita awamu mpya katika vita hivyo. Afisa huyo wa Ukarine alikisia kwamba vita hivyo vinaweza kudumu kwa muda mwingine wa miezi miwili hadi sita, kulingana na wingi wa silaha zilizokusanywa. Podoliak pia amedai kuwa vifo na majeruhi vya wanajeshi wa Urusi sasa vimepungua na kufikia 100 hadi 200. Ameongeza kuwa takwimu hiyo inaweza kulinganishwa na ya Ukraine. Podoliak ameongeza kuwa mwanzoni mwa vita hivyo, vikosi vya Urusi vilikuwa havielewi wanachkifanya lakini sasa hilo limebadilika. Urusi ilianzisha vita nchini Ukraine takriban siku 100 zilizopita. Vikosi vya Urusi vilionekana kuweka nguvu kwenye mashambulizi katika eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine.