Meya wa mji wa Sloviansk, Vadym Liakh amewataka wakaazi wa eneo hilo kuondoka, kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi ya vikosi vya jeshi la Urusi. Liakh amesema mashambulizi ya jana ya Urusi, yameharibu mifumo ya umeme kwenye mji huo ulioko katika jimbo la Donetsk mashariki mwa Ukraine. Akizungumza kupitia mtandao wa mawasiliano wa Telegram, meya huyo amesema mji huo hauna umeme na usambazaji wa maji uko chini, na kwamba suluhisho la haraka katika hali hii ni watu kuondoka. Shirika la habari la AFP limewanukuu watu walioshuhudia wakisema kwamba siku ya Jumanne mashambulizi ya Urusi yaliwaua watu watatu na kuwajeruhi wengine sita katika mji wa Sloviansk. AFP imeripoti kuwa wakaazi wa mji huo jana jioni walikuwa wakipanda kwenye mabasi madogo matano yaliyotengwa kwa ajili ya kuwahamisha watu.