Imetimia siku 100 tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, Februari 24, wakati huu mashambulio yakiendelea katika jimbo la Donbas kwa lengo la kuteka eneo lote la Mashariki.
Mpaka sasa rais Volodymyr Zelensky amesema, wanajeshi wa Urusi, wamedhibiti asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine na ameendelea kutoa wito kwa washirika wa nchi hiyo, kuendelea kuisaidia.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza, imesema lengo la Urusi kuuteka mji mkuu Kiev umeshindikana na sasa Moscow, imeweka nguvu zake, Mashariki mwa Ukraine na inaelekea kuudhibiti mji wa Luhansk ndani ya wiki mbili zijazo.
Ripoti zinaeleza kuwa hali inaendelea kuwa mbaya katika mji wa Severodonetsk, ambao unashuhudia mapigano makali na jeshi la Urusi linaendelea kutekeleza uharibu mkubwa.
Urusi iliishambulia Ukraine kwa madai kuwa, ilikuwa inafanya operesheni maalum, kwa lengo la kulinda usalama wake baada ya kuishtumu jirani yake kuwa na silaha hatari na ilikuwa na mpango wa kujiunga na jeshi la nchi za Magharibi NATO.
Hata hivyo, mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani na Umoja wa Ulaya, yanasema, lengo la uvamizi huu, ni kuifuta kabisa nchi ya Ukraine na jitihada za kujaribu kutafuta suluhu ya kidiplomasia ili kusitisha vita, inaonekana kugonga mwamba.
Wiki hii, Marekani imetangaza vikwazo zaidi dhidi ya Urusi, huku ikitangaza silaha zaidi za kijeshi kwa Ukraine, kuisaidia katika mapambano dhidi ya Urusi.
Mamilioni ya watu nchini Ukraine wameikimbia nchi yao tangu kuanza kwa vita hivyo, pamoja na maafa ya wananchi pamoja na wanajeshi wa Ukraine na Urusi.