Machafuko yazuka Jerusalem kufuatia mazishi

Polisi wa Israel walifyetua gesi ya kutoa machozi na risasi za mpira kuyatawanya makundi ya waandamanaji Wapalestina jana Jumatatu kufuatia machafuko yaliyotokea baada ya mazishi ya kijana wa Kipalestina aliyekufa kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa makabiliano na polisi mwezi uliopita. Shirika la Hilal nyekundu la Palestina limesema watu 52 walijeruhiwa na risasi za mpira, maguruneti na kipigo. Watu wengine 12 walilazwa wakiwemo wawili waliojeruhiwa kwenye macho. Polisi ya Israel imesema maafisa wake kadhaa walipata majeraha madogo. Mamia ya waombolezaji walijiunga na msafara wa mazishi ya Waleed Shareef aliyefariki Jumamosi iliyopita na kuupeleka kwa sala katika msikiti wa Al-Aqsa kabla kuelekea makaburini nje ya mji mkongwe. Polisi wa Israel wanasema waandamanaji waliwarushia mawe, vijiti na vilipuzi maafisa wa usalama.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii