Mashambuli ya makombora yaharibu miundo mbinu ya kijeshi Ukraine

Gavana wa jimbo la Lviv nchini Ukraine Maxim Kozitsky amesema leo kuwa mashambulizi manne ya makombora yamelenga miundo mbinu ya kijeshi katika eneo la Yavoriv Magharibi mwa Ukraine karibu na mpaka na Poland leo asubuhi. Katika ujumbe kupitia mtandao wa Telegram, Kozitsky amesema kuwa miundombinu hiyo imeharibika kabisa. Awali, mamlaka ya kijeshi ya kanda nchini Ukraine ilisema kuwa makombora kadhaa yalirushwa katika eneo hilo la Lviv kutoka bahari nyeusi katika masaa ya alfajiri ya leo Jumapili. Wakati huo huo, vikosi vya Urusi vimeanza kuondoka katika viunga vya jiji la pili kwa ukubwa nchini Ukraine la Kharkiv, ikiwa ni baada ya kuushambulia vibaya mji huo kwa majuma kadhaa. Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa jeshi la Ukraine ambalo limesema pia majeshi hayo kwa sasa yanaongeza mashambulizi yake katika eneo lenye viwanda vingi la mashariki mwa nchi hiyo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii