Niger yasema imeuwa wanamgambo 40 wa Boko Haram

Serikali ya Niger inasema jeshi lake limewauwa wapiganaji 40 wa kundi la Boko Haram kwenye mapigano katika visiwa vya Ziwa Chad. Wizara ya ulinzi ya Niger imesema usiku wa Jumatano, wapiganaji wapatao 100 wa kundi hilo waliwasili wakiwa na mitumbwi minne na boti moja ya kivita na kujaribu kuvishambulia vikosi vya wanajeshi katika visiwa vya Ziwa Chad, ambalo linaziunganisha Niger, Nigeria, Cameroon na Chad. Kwa mujibu wa wizara hiyo, makabiliano yaliyozuka baina ya pande hizo mbili yalisababisha vifo wa wapiganaji 40 wa Boko Haram, pamoja na kutekwa kwa idadi kubwa ya silaha zao. Bonde la Ziwa Chad lenye visiwa kadhaa limekuwa ngome kuu ya kundi hilo la kigaidi kwa muda mrefu sasa, ambalo ni sehemu ya kundi lijiitalo Dola la Kiislamu la Afrika Magharibi, ISWAP. Niger, Nigeria, Cameroon na Chad ziliunda kikosi cha pamoja mwaka 2015 kukabiliana na kundi hilo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii