Afisa wa polisi auawa Pakistan, wafuasi wa Khan wakamatwa

Chama kikuu cha upinzani nchini Pakistan Tehreek-e-Insaf kinachoongozwa na waziri mkuu aliyeondolewa madarakani hivi karibuni Imran Khan, kimeishtumu polisi kwa kuwazuilia mamia ya wafuasi wake katika misako iliyoanza mapema leo. Afisa mmoja wa polisi aliuawa wakati wa moja ya misako hiyo wakati mmoja wa wafuasi wa Khan alipofyetua risasi. Fawad Chaudhry, msemaji wa chama hicho, amesema kuwa polisi ilianzisha operesheni hiyo muda mfupi baada ya saa sita usiku hapo jana. Kufikia leo asubuhi, msako bado ulikuwa unaendeshwa dhidi ya makazi ya wafuasi wa chama hicho na takriban wafuasi 400 kukamatwa kote nchini humo. Katika ujumbe kupitia mtandao wa twitter, Khan amelaani kukamatwa kwa wafuasi wake. Mamlaka nchini humo imethibitisha kufanyika kwa misako hiyo lakini haikutoa habari zaidi kuhusu kukamatwa kwa wafuasi hao.Waziri wa masuala ya ndani Rana Sanaullah, amemshtumu Khan kwa kutafuta kuanzisha hali kama ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii