Mkuu wa Shirika lenye kuwahudumia wakimbizi duniani, UNHCR Filippo Grandi amesema wa mara ya kwanza vita vya Ukraine vimeongeza idadi ya watu waliolazimishwa kuyakimbia makaazi yao duniani na kupindukia milioni 100.Mkuu huyo amesema hali hiyo lazima iwe kama tahadhari ya kutatua na kuzuia migogoro yenye kusababisha uharibifu, kukomesha mateso na kushughulikia vyanzo vinavyochangia watu wasio na hatia kuyakimbia makazi yao.Takwimu kutoka shirika hilo la Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa idadi ya watu waliokimbia makwao ilikuwa imefikia milioni 90 mwishoni mwa mwaka 2021. Lakini uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umesababisha watu milioni nane kuwa wakimbizi wa ndani na wengine zaidi ya milioni sita kukimbilia nje ya nchi. Mbali na wakimbizi wa Ukraine kupokelewa vyema na mataifa ya Magharibi, Grandi amesema michango kwa mashirika yanayowasaidia wakimbizi kwa ujumla imeshuka duniani.