Mawaziri Dkt. Dorothy Gwajima wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Hamadi Masauni
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, wameuambia umma kuwa, vijana wadogo
wanaovamia watu na kuwakata kwa silaha zenye ncha kali kisha kuwa pora
hawana uwezo wa kushindana na serikali iwapo wananchi watakuwa bega kwa
bega katika kutoa taarifa za Uhalifu na viashiria kwa mamlaka za
Serikali.
Wakizungumza hapo jana, Mei 18, 2022, Jijini Dar es
Salaam kwenye kata za Chanika, Zingiziwa na Buza jijini humo wamesema,
uwepo wa Mshikamano wa wanajamii na Serikali ndio suluhu ya kutokomeza
vikundi hivyo vya vijana wanakadiriwa kuwa na miaka kati 16 hadi 20
kiasi.
Akizungumza kwenye Mkutano wa Hadhara, Waziri wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima,
alisema kumomonyoka kwa maadili katika makuzi na malezi ndio chanzo
kikuu cha uzalishaji wa Kundi hilo.
“Mpaka mtoto anakuwa hivyo,
sio suala la usiku mmoja, unakuta anaanza kidogo kidogo na ninyi wazazi
kwakuwa hamtengi muda wakuzungumza naye na kujua mienendo yake, anazidi
kukuwa na tabia hiyo hadi anafikia hatua sasa yakujiunga kwenye makundi
ya kihalifu kama hilo la Panya Road” alisema Dkt. Gwajima
Waziri
Gwajima, ameonya baadhi ya wanajamii kuacha kumuangalia mtoto kwa niwa
mtu mwingine na badala yake watoto wote wahesabike kuwa wanajamii, kwani
katika malezi ya sasa, baadhi ya wazazi hupandwa na hasira mwanae anapo
adhibiwa au kuonywa na mzazi mwingine hali inayo nyong’onyeza jitihada
za malezi na makuzi.
“Yapata juma moja nilikuwa eneo la Mbezi
Luis, wazazi waliweka bayana haya mambo, wakisema, malezi ya zamani
yalishirikisha jamii nzima, lakini kwa nyakati za sasa, wazazi wengi
huweza kukufokea pale unapojaribu kumuongoza mwanane kwenye maadili
mema, hii sio sawa kwani kufanya hivyo, huyo huyo mwanao Pamoja na wewe
kujenga Gorofa kutokana na kutokuwa na malezi bora Mwanao mwenyewe
anaweza kukuchinja kwenye nyumba yako. Alisisitiza Dkt. Gwajima.
Naye
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamadi Masaun, akiongea kwenye Mkutano
huo ambao pia ulishirikisha Viongozi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, alisema amefarijika kusikia tayari vijana zaidi ya 61 wakiwa
wanashikiliwa na jeshi la Polisi kutokana na Ushirikiano ulioneshwa na
Jamii.
“Mwanzoni nilipokuja hapa kila mmoja wetu alikuwa na sura
ya simanzi kutokana na hofu na woga ulikuwa umetanda, lakini leo
mmeniambia tayari wapo ambao wanashikiliwa na vyombo vya dola, lakini
wengine tayari wamefikishwa Mahakamani kwa ajili yakukabiliana na kesi
zao, niwapongeze sana kwa hili” alisema Masauni.
Naye Kamanda wa
Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alisema, kama
Jeshi la Polisi kwenye Kanda hiyo wataendelea kufanya kazi kwa mujibu wa
viapo vyao na hawata muonea muhali mtu yeyote ambaye atathubutu kucheza
na Amani ya Mtanzania yeyote kwenye kanda hiyo.
“Tumefanya kazi
kwa ukaribu sana na Polisi Jamii, hawa wamekuwa msaada mkubwa na
kutuwezesha kuwapata baadhi ya wahalifu hao katika maeneo ya Chanika,
Kunduchi Mtongani na Nyatira, ambapo baadhi ya watu waliokamatwa
walikutwa na TV, Simu na vitu vingine vilivyo porwa kwenye matukio
hayo.” Alisema Kamanda Muliro.
Nao wananchi wa Maeneo ya Chanika
na Kata ya Buza hawakusita kuonesha furaha yao baada yakuwaona Mawaziri
hao huku wakiwasifu na kumshukuru Waziri Gwajima kwa darasa la kamati za
MTAKUWWA na majukumu yake.
Mawaziri Dkt. Gwajima na Masauni, kwa
Pamoja na Kamanda wa Polisi kanda Maalum ya Dar es Salaam, walifanya
ziara kwenye Kata za Chanika, na Buza na kuongea na wahanga wa matukio
ya Panya Road yaliyokithiri kwenye jiji hilo ndani ya majuma mawili
yaliyopita.