Watu watano wamekufa baada ya ghorofa kuporomoka Nigeria

Watu watano wamekufa usiku wa kuamkia leo baada ya jengo moja la ghorofa tatu kuporomoka kwenye mji wa kibiashara wa Nigeria wa Lagos na kuna wasiwasi watu wengine kadhaa wamekwama chini ya kifusi cha jengo hilo. Mkuu wa Idara ya taifa ya matukio ya dharura Ibrahim Farinloye amesema hadi sasa watu 23 ikiwemo watoto 7 tayari wameokolewa huku 9 kati ya hao wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani. Wakaazi wa eneo ambako mkasa umetokea wamejiunga na vikosi vya uokozi kuwatafuta manusura kutoka kwenye kifusi lakini bado haijafahamika ni watu wangapi walikuwemo kwenye jengo hilo wakati lilipoanguka. Matukio ya kuporomoka kwa majengo hutokea mara kwa mara nchini Nigeria hususan kwenye mji wa Lagos ambako mwaka uliopita majengo matano ya roshani yalianguka.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii