Upinzani uliogawika Sri Lanka waungana kumtaka rais aondoke madarakani

Upinzani uliogawika nchini Sri Lanka hapo jana umeonyesha mshikamano wa nadra ulipoungana na kumtaka Rais Gotabaya Sajapaksa kujiuzulu kufuatia mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi ulioikumba nchi hiyo. Haya yamefanyika baada ya chama kikuu cha upinzani Samagi Jana Balawegaya SJB kufanya maandamano makubwa katika Mji Mkuu Colombo ambapo wasemaji wote walimtaka rais Rajapaksa na familia yake yenye nguvu kuondoka uongozini. Chama cha mrengo wa kushoto cha JVP nacho kilifanya mkutano wake wa kisiasa katika kituo cha treni cha Colombo na kumtaka kiongozi huyo ang'atuke madarakani na kutoa nafasi ya kufanyika uchaguzi wa mapema. Miezi kadhaa ya ukosefu wa umeme, mfumuko wa bei unaoongezeka na ukosefu mkubwa wa chakula, mafuta na madawa ni mambo yaliyochochea maandamano kadhaa ya kumpinga rais huyo kote nchini Sri Lanka.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii