Mexico yamkamata kiongozi wa kundi lenye nguvu la wauza madawa ya kulevya

Mamlaka ya Mexico imemkamata kiongozi anayeshukiwa kuwa wa kundi lenye nguvu la wauza madawa ya kulevya la Jalisco New Generation. Francisco Javier Rodriguez Hernandez, anayejulikana kama "El Senoron" au "XL", alikamatwa siku ya Ijumaa katika mji wa kitalii wa Mazatlan, kaskazini-magharibi mwa jimbo la Sinaloa, katika operesheni iliyofanywa na maafisa wa jeshi la wanamaji. Kulingana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Morelos, Rodriguez Hernandez, ambaye anadaiwa kuongoza kundi la CJNG katika jimbo hilo la katikati mwa Mexico, alisakwa kwa mauaji, yakiwemo ya madaktari watatu mnamo Aprili mwaka 2020. Julai mwaka jana, mamlaka ilitoa zawadi ya dola 25,000 kwa habari zitakazowezesha kukamatwa kwake. Mexico imenaswa katika msururu wa machafuko yanayohusiana na biashara ya madawa ya kulevya ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 340,000 tangu mwaka 2006.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii