Machafuko yazuka upya Al Aqsa Jerusalem

Machafuko yamezuka upya hii leo kati ya Wapalestina na polisi wa Israel katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem na watu 40 wamejeruhiwa 22 kati yao wakihitaji matibabu. Shirika la Hilali Nyekundu limeripoti juu ya tukio hilo wakati kwa upande mwingine polisi ya Israel imesema maafisa waliingia eneo la msikiti huo baada ya Wapalestina waliokuwa wakifanya fujo kurusha mawe na baruti kuelekea Ukuta wa Magharibi ambalo ni eneo takatifu la Wayahudi liliko upande wa chini wa msikiti wa al Aqsa. Taarifa ya Israel imeeleza kwamba maafisa walitumia njia za kuzuia fujo kudhibiti machafuko. Mashahidi na waandishi wa habari wa shirika la AFP wamesema polisi walifyetua gesi ya kutowa machozi na risasi za mpira. Mapambano hayo yalitulia kufuatia sala ya asubuhi kwa mujibu wa mashahidi na waandishi habari, ingawa bado kuna hali ya wasiwasi mkubwa katika eneo hilo. Machafuko hayo mapya pia yanatokea wakati ambapo Waislamu wanaadhimisha Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhan unaomalizika mwanzoni mwa wiki ijayo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii