Urusi imeyashambulia kwa makombora maeneo kadhaa ya maakazi kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa ziarani kwenye mji huo. Guterres na ujumbe wake hawajapata madhara yoyote lakini taarifa zinasema kuna raia wa Ukraine waliopoteza maisha. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema mashambulizi hayo ni sehemu ya juhudi za watawala wa Urusi kuudhalilisha Umoja wa Mataifa. Wakati huo huo waendesha mashtaka nchini Ukraine wamesema wamewatambua wanajeshi 10 wa Urusi wanaoshukiwa kufanya uhalifu wa kivita kwenye mji wa Bucha. Hatua hiyo ni sehemu ya uchunguzi mpana unaolenga hapo baadae kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wote waliohusika na vitendo vya kikatili katika vita vya Ukraine.