Mariam Nabatanzi alikuwa na umri wa miaka 13 tu alipojaaliwa pacha wake wa kwanza. Na wakati anafikisha umri wa miaka 36, tayari Mariam alikuwa amejifungua watoto wengine 42, ambao inambidi awalee peke yake baada ya mume wake kuitoroka familia hiyo kubwa.
Alipofikia umri wa miaka 43, aliambiwa kuwa ana tatizo la kijeni lisilo la kawaida, ambalo linamaanisha kwamba aliendelea kuzaa pacha - licha ya kuomba msaada wa madaktari kumsaidia alipokuwa na umri wa miaka 23 pekee.
Mariam ana seti tatu za watoto wanne, seti nne za mapacha watatu na seti sita za mapacha wawili na amejaaliwa uwezo wa ajabu wa kuwatunza na kuwalisha wote peke yake.
Mama huyo mwenye rotuba tele alikuwa na umri wa miaka 12 tu alipoolewa na mume wake, ambaye akiwa na umri wa miaka 40, tofauti ya miaka 28 ilikuwa kubwa kwake.
Mwaka mmoja tu baadaye alijifungua seti yake ya kwanza ya mapacha.
Sasa, yeye na watoto wake wote hawana budi kuishi katika hali duni ya kutisha katika nyumba nne ndogo zilizotengenezwa kwa matofali ya saruji na paa la bati. Mariam, kutoka Uganda, na watoto wake wanaishi huku kuzungukwa na mashamba ya kahawa.
Daktari alimwonya mama huyo kwamba udhibiti wa uzazi, kama vile Kidonge, ungeweza kumsababishia matatizo kwa sababu alikuwa na ovari kubwa isivyo kawaida.
Kwa hivyo baada ya seti yake ya kwanza ya mapacha, watoto waliendelea kuja.Familia za Uganda mara nyingi ni kubwa huku wanawake wakiwa na watoto 5.6 kwa wastani.
Hii ni miongoni mwa viwango vya juu zaidi vya uzazi barani Afrika lakini hata kwa viwango hivi, familia ya Mariam ni kubwa sana. Akiwa na umri wa miaka 23 tu, Mariam alikuwa na watoto 25 na alimwomba daktari wake amsaidie kuzuia asizae tena.
Lakini kwa mara nyingine ushauri wa kimatibabu ulikuwa kwamba aendelee kutungwa mimba kwa sababu idadi ya ovari zake ilikuwa ya juu sana.
Mimba ya mwisho ya Mariam miaka minne iliyopita iliishia kuwa msiba alipojifungua watoto wake mapacha wa seti ya sita. Mmoja wa watoto hao aliaga dunia alipokuwa katika uchungu wa kujifungua, kisha mume wake, ambaye mara nyingi aliondoka kwa majuma kadhaa kabla ya kurejea, akamwacha kabisa.
Mariam alisema: “Nimekua kwa majonzi mengi, mume wangu amenipitishia kwenye mateso mengi.
"Wakati wangu wote nimeutumia kuwatunza watoto wangu na kufanya kazi ili kupata pesa."
Lakini pia ni baada ya mimba hii ambapo mama huyu hatimaye alipata msaada wa kimatibabu aliohitaji kumzuia kuendelea kuzaa zaidi.
Dkt. Charles Kiggundu, daktari wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Mulago huko Kampala, Uganda, alisema: "Kisa chake ni mwelekeo wa jeni kuwa na uwezo mkubwa wa kuotesha mayai mengi katika mzunguko mmoja, ambayo huongeza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kuzaa pacha kwa wingi; daima ni maumbile. "
Mariam alithibitisha kuwa madaktari walichukua hatua kuondoa hatari ya kupata ujauzito tena.
Alisema daktari alimwambia "amekata uterasi yangu kutoka ndani".
Hakuna cha kumzuia mama huyu aliyejitolea kufanya yote awezayo kuwaruzuku watoto wake. Anafanya kazi ya kusuka nywele, mpambaji wa hafla na hukusanya na kuuza vyuma chakavu.
Mariam pia hutengeneza pombe yake ya kienyeji ili kuuza na kutengeneza dawa za mitishamba. Mariam ana kazi nyingi na anafanya yote awezayo kusaidia familia yake kubwa
Na amedhamiria kuwa watoto wake waliobakia watakuwa na mwanzo bora wa maisha huku sehemu kubwa ya mishahara yake ikiitumia kwa chakula, matibabu, nguo na karo za shule. Picha zinazoning'inia kwenye ukuta wa nyumba yake ndogo ni za watoto wake wakubwa wakihitimu masomoni.
Licha ya juhudi kubwa za Mariam, mtoto wake mmoja, Ivan Kibuka, alilazimika kuacha shule ili kusaidia kulea familia yao.