Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa jamii kutonyamazia matukio ya ukatili wa kijinsia na badala yake watoe taarifa za wahusika wa matikio hayo ili wachukuliwe hatua stahiki.
Waziri Mkuu ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa papo , baada ya Mbunge wa viti maalum CCM kutoka mkoa wa Tanga , Mwantumu Zodo kutaka ufafanuzi kuhusu mkakati wa Serikali katika kukabiliana na ongezeko la matukio ya unyanyasaji wa kijinsia, ukatili na mauaji ya Wanawake na Watoto.
Pia amejibu swali la Mbunge wa jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro Saashisha Mafuwe aliyetaka Serikali itoe kauli kuhusu Wanafunzi waliorudi nchini kutoka masomoni nje ya nchi kutokana na vita au janga la UVIKO 19.
Waziri Mkuu amewasisitiza Wanafunzi hao kuripoti Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili waelekezwe utaratibu utakaowawezesha kuendelea na masomo yao wakiwa Tanzania na kupata mwongozo wa kozi walizokuwa wanasoma.