Urusi yaulenga mji wa Odesa kwa makombora

Ukraine imesema leo kuwa vikosi vya Urusi vimeishambulia bandari muhimu ya mji wa Odesa katika juhudi za karibuni kabisa za kuhujumu mifumo ya usambazaji wa bidhaa na upokeaji silaha kutoka mataifa ya magharibi. Maafisa wa Ukraine wamearifu kwamba Urusi imeulenga mji wa Odesa kwa makombora saba yaliyosababisha kifo cha mtu na kuharibu kituo cha biashara pamoja na ghala kwenye viunga vya bandari ya mji huo ambayo ndiyo kubwa zaidi nchini humo. Meya wa mji wa Odesa Gennady Trukhanov, amelitembelea eneo la bandari ikiwemo ghala lililoharibiwa na kusema halikuwa sehemu ya kituo cha kijeshi wala halikutumika kuhifadhi silaha au vifaa vyovyote vya kijeshi. Moscow imekuwa ikiyashambulia maeneo ya mashariki mwa Ukraine ikilenga kulikamata jimbo la Donbas na bandari kwenye bahari Nyeusi na ile ya Azov tangu ilipoondoa vikosi vyake karibu na mji mkuu wa Ukraine, Kyiv wiki kadhaa zilizopita.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii