Iran inadai inauza nje mafuta mengi licha ya vikwazo vya Marekani

Rais wa Iran Jumatatu amesema nchi yake inauza nje mafuta mara mbili zaidi ya wakati alipoingia madarakani mwezi Agosti, na licha ya vikwazo vikali kwa mauzo ya mafuta ya Iran vilivyowekwa na Marekani.

Ebrahim Raisi ametoa madai hayo katika mahojiano ya moja kwa moja kwenye kituo cha televisheni ya taifa bila kufafanua zaidi, au ni kiwango gani cha mafuta yanayouzwa nje.

“Mauzo ya mafuta yameongezeka maradufu, hatuna wasiwasi kuhusu mauzo ya mafuta,” amesema.

Matamshi ya Raisi yanajiri wakati masoko ya kimataifa yanatafuta njia nyingine za kununua mafuta ghafi yasiyotoka Russia kufuatia uvamizi wa Moscow dhidi ya Ukraine na vikwazo vya nchi za magharibi dhidi ya Russia.

Mafuta ghafi ya Iran, yenye vigezo sawa na mafuta ghafi ya Russia, yanashindana kwenye soko la kimataifa la mafuta.

Kama athari za vita vya Ukraine na changamoto za usambazaji wa mafuta, bei ya mafuta ilipanda kwa viwango vya juu sana tangu miongo kadhaa.

Bei ya kimataifa ya mafuta ghafi ilifikia dola 140 mwezi Machi kwa pipa moja. Pipa moja la mafuta ghafi lilikuwa linauzwa dola 105 Jumatatu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii