Watu kadhaa wauwawa na waasi mashariki mwa Congo

Watu kadhaa wameuwawa na wengine wengi hawajulikani waliko baada ya wanaume waliokuwa wamejihami na silaha kuivamia kambi ya uchimbaji madini karibu na mji wa Mongwalu katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Viongozi wa mashirika matatu ya kiraia wamekadiria watu kati ya 30 na 50 wameuwawa katika uvamizi huo wa jana Jumapili. Dieudonné Lossa anayeongoza muungano wa mashirika ya kijamii amewanyoshea kidole cha lawama waasi wa kundi la CODECO, ambao wamejijengea sifa kwa kuyashamulia maeneo ya umma. Msemaji wa jeshi Jules Ngongo Tsikudi amethibitisha kutokea kwa shambulizi hilo la umwagaji damu lakini hakutoa maelezo kuhusu idadi ya watu waliouwawa. Tsikudi aidha amesema wanafuatilia kufahamu idadi kamili ya vifo katika saa chache zijazo na jeshi lifanya kazi usiku na mchana kuyachakaza kabisa makundi ya waasi mkoani Ituri.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii