Zaidi ya watu 10,000 wamekimbia mapigano kati ya jeshi la Iraq na wapiganaji wa Yazidi wenye mafungamano na chama cha wafanyikazi cha Kurdistan PKK kilichopigwa marufuku nchini Uturuki. Afisa kutoka eneo la Kurdistan nchini Iraq amesema idadi hiyo ni zaidi ya mara mbili iliyoripotiwa katika eneo hilo mnamo siku ya Jumanne. Mapigano yalisababisha kifo cha mwanajeshi mmoja wa Iraq siku ya Jumatatu katika eneo la kaskazini la Sinjar, eneo la Yazidi walio wachache ambamo hutokea makabiliano ya mara kwa mara kati ya vikosi vya usalama na wapiganaji wa Yazidi wenye mafungamano na PKK. Mapigano ya hivi karibuni yamesababisha watu kukimbilia eneo la Kurdistan, huku wengine wakielekea katika jimbo la Dohuk. Wayazidi ni jamii ya walio wachache wasio waarabu na wanaozungumza Kikurdi, waliuawa kinyama na wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu mnamo mwaka 2014.