Hamas yasema bado mapambano yanaendelea Gaza

Kiongozi wa kundi la Hamas katika ukanda wa Gaza, Ismail Haniya ametishia kuzidisha makali ya mapigano kati ya kundi hilo na Israel baada ya pande zote mbili kwa mara nyengine kurushiana makombora usiku kucha.

Wanamgambo hao wa Ukanda wa Gaza walirusha maroketi yaliyoulenga mpaka wa Israel Jana jioni na mapema leo alfajiri. Ving'ora vya kuashiria hali ya hatari vilisikika mara mbili Kusini mwa Israel hii ikiwa ni kulingana na jeshi la taifa hilo. Israel nayo ilijibu kwa kuyashambulia mahandaki yenye vituo vya Hamas vya kutengeneza maroketi kwa nia ya kupunguza uwezo wa wapalestina kutengeneza silaha hizo.

Pande zote mbili zimekuwa katika mapigano makali wiki hii wakati wanajeshi wa Israel walipopambana na raia wa palestina katika eneo takatifu la Jerusalem. Watu kadhaa wamejeruhiwa katika mapambano hayo hali inayozidisha mvutano kati ya pande hizo mbili hasa wimbi la mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya wapalestina.

Machafuko hayo kwenye mpaka wa Gaza, yanaonekana kuwa mapigano makubwa zaidi tangu vita vya mwaka jana wakati wa mfungo wa Ramadhani vilivyodumu kwa siku 11 na yanakuja licha ya kuwepo juhudi za kuzuia marudio ya vita hivyo.

Israel imesema inawanyooshea kidole cha lawama Hamas kwa matukio yote inayoyaita ya kigaidi yanayoilenga ardhi ya Israel kutoka ukanda wa Gaza.

Hata hivyo kundi la Hamas kupitia kiongozi wake Ismail Haniya limesema ndio mwanzo limeanza mapambano na lina imani ya kushinda ilichokitaja kuwa ''sera ya uvamizi''.

Polisi ya Israeli imesema waandamanaji waliofunika nyuso zao walikusanyika katika msikiti wa Al Aqsa wakafunga mlango na kuanza kurusha mawe na mabomu ya petroli. Polisi hiyo iliongeza kuwa ilijaribu kuwatawanya waandamanaji hao wa kipalestina kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi. Kulingana na shirika la hilali nyekundu watu 20 walijeruhiwa na mwengine mmoja kuwa katika hali mahututi.

Eneo la msikiti wa Al Aqsa ndio kitovu cha vurugu kati ya waumini wa dini ya kiislamu na ya Kiyahudi. Msikiti huu ni eneo muhimu la tatu lililotakatifu kwa waumini wa kiislamu na  ni eneo takatifu zaidi kwa Wayahudi.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii