JELA MIAKA 20 KWA KUWAPIGA WAFANYAKAZI WAKE.

Mahakama nchini Rwanda imemhukumu kifungo cha miaka 20 Mchina aliyetambuliwa kwa jina la Shujun Sun baada ya kupatikana na hatia ya kuwatesa wafanyakazi wake
Mchina huyo aliyedai kuwa wafanyakazi hao walikuwa wameiba madini yake, alikamatwa mara moja Jumanne, Aprili 19, kutumikia kifungo chake katika Gereza la Rubavu.
Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya Igihe ya Rwanda, Shujun alishtakiwa pamoja na Alexis Renzaho, mhandisi aliyekuwa akisimamia shughuli za uchimbaji madini na Leonidas Nsanzimana, mlinzi.
Shujun Sun na washtakiwa wengine wawili walirejeshwa rumande mnamo Septemba 21, 2021, na Mahakama ya Gihango lakini washtakiwa hao walikata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Mahakama ya Karongi ilimwachilia Shujun kwa dhamana mnamo Oktoba 14, 2021 huku akipokonywa pasipoti yake.
Aitisha mkutano
Mchina huyo aliitisha mkutano baada ya kushuku watu wameiba madini yake.
Kisha alitoa onyo kuwa yeyote atakayepatikana akizurura karibu na mgodi wake au anayeshukiwa kuiba atapigwa mahali paitwapo Golgotha, ambapo alisimamisha msalaba.
Mchina huyo alitumia mbao kutoa adhabu ya viboko kwa vijana wawili wanaoshukiwa kuiba ambao aliwafungwa kwenye mbao kwa kamba huko Nyamasheke.
Kwa kuzingatia ushahidi uliopo, Mwendesha Mashtaka aliiomba mahakama kutoa kifungo cha miaka 20 kwa Shujun Sun.
Mahakama pia iliamuru kwamba Shujun Sun na Renzaho watalipa fidia ya thamani ya Rwf2.5 milioni (KSh 283,210) kwa kila mwathiriwa na pia kuwalipa mawakili wa walalamishi.
Shujun Sun na Renzaho wamepewa mwezi mmoja kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii