Ndege iliyokuwa imebeba abiria 60 ikitokea Nairobi kuelekea Uganda, iliteleza na kutoka kwenye njia yake ilipokuwa ikitua katika uwanja wa ndege wa Entebbe mnamo Jumatano, Aprili 20 asubuhi.
Ndege hiyo ya Shirika la RwandaAir, ilianza safari yake mjini Kigali, Rwanda, kabla ya kusimama Nairobi.
Gazeti la Daily Monitor nchini Uganda, limeripoti kuwa abiria 20 kati ya 60 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walikuwa wameratibiwa kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa kwa mwanawe Rais Yoweri Museveni, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Wanawake hao 20 kutoka Rwanda ni akiwemo mshindi wa zamani wa urembo nchini Rwanda, Jolly Mutetsi ambao walikuwa wamealikwa kuhudhuria karamu ya kuadhimisha miaka 48 ya Muhoozi, itakayofanyika Jumapili.
Shirika hilo la ndege limetoa taarifa kuthibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa hakuna majeruhi walioripotiwa.
"Tunaweza kuthibitisha kuwa safari ya ndege ilihusika katika tukio la saa 05:31 asubuhi ya leo, ambalo lilipelekea ndege hiyo kuacha njia ilipotua Entebbe wakati wa hali mbaya ya hewa."
"Wateja wote na wafanyakazi walihamishwa salama, na hakuna majeraha yaliyoripotiwa. Hali imedhibitiwa na tunawasiliana na wateja walioathirika. Ndege kwa sasa inarejeshwa, kwa hivyo njia ya kurukia ndege ya Entebbe inaweza kurudi kutumika," taarifa hiyo ilisema kwa sehemu.