Ukraine imeapa kupambana hadi dakika ya mwisho katika mji uliozingirwa wa Mariupol baada ya kumalizika kwa muda uliowekwa na Urusi kwa kuwataka wapiganaji wake kuweka chini silaha na kujisalimisha.Waziri mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal amesema saa kadhaa tayari zimepita tangu kumalizika kwa muda wa mwisho uliowekwa na Urusi lakini hadi sasa vikosi vya Ukraine havijasalimu amri na vitaendelea kupambana.Mapema jana Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alisema mazungumzo ya amani kati ya nchi yake na Urusi yatasitishwa iwapo Moscow itawaua wanajeshi waliosalia kwenye mji wa Mariupol.Jeshi la Urusi ambalo sasa limehamishia nguvu zake kwenye kuchukua udhibiti wa jimbo la Donbas limesema kuna wapiganaji wachache wa Ukraine waliobakia ndani ya mji wa Mariupol na jana iliwataka kujisalimisha kwa ahadi ya kutowashambulia.