Wakati mgogoro ukizidi kufukuta kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde, leo baadhi ya waumini wa usharika wa Mbalizi wamemzuia mchungaji wao, Atupele Mlawa kuingia kanisani na kusababisha kuvunjika kwa ibada.
Kutokana na vurugu hizo, Jeshi la Polisi mkoani humo limefika kanisani hapo na kukamata baadhi ya viongozi wa kanisa hilo.
Vurugu hizo zimetokea leo Jumapili Aprili 17 wakati Wakristo kote duniani wakisherekea siku kuu ya Pasaka.
Baadhi ya waumini waliozungumza na Mwananchi kanisani hapo wamesema vurugu zilianza baada ya baadhi ya waumini kufunga milango kumzuia mchungaji Mlawa kutoingia ndani kuendesha ibada wakidai kutumia vibaya mali za kanisa hilo.
Taarifa zaidi zimesema waumini wanaompinga Mchungaji Mlawa, wanamtaka Mchungaji Lusajo Sanga aliyechaguliwa hivi karibuni kwenye uchaguzi uliofanyika Machi 22 chini ya Kiongozi wa Kanisa hilo nchini, Dk Fredrick Shoo.
Hata hivyo, waumini wengine walipinga kitendo cha kufunga milango ya kanisa wakitaka mchungaji Mlawa aendelee na kazi yake na ndipo vurugu zilipozuka.
Akizunguka katika eneo la kanisa hilo, mmoja wa waumini, Jane Msingwa amesema baadhi ya waumini walisimama mlangoni wakipinga mchungaji Mlawa kuingia kanisani.
"Leo kilichotokea ni sintofahamu, mchungaji alikuja kuendesha ibada lakini watu wakakaa mlangoni hadi msaidizi wake akaingilia kati ila hali ilikuwa mbaya," amesema Jane.
Kwa upande wake Godfrey Mwasuku amesema wameamua kukaa mlangoni hapo kutokana na kukaidi kwa mchungaji huyo maelekezo kwani alishaandikiwa barua ya kuondoka kanisani hapo.
"Hiki kilichotokea leo ni kutokana na uongozi tulionao, ilipangwa ratiba ya ibada na huyu mchungaji Mlawa tulishamuandikia barua kuondoka, imeshangaza tunamuona amekuja ndio maana tukasema hatumtambui," amesema Mwasuku.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Ulrich Matei amesema baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa vurugu aliwatuma askari wake kwenda kumaliza mzozo.
"Msimamo wetu Jeshi la Polisi tumewaambia hao viongozi tuliowakamata nini cha kufanya, waende mahakamani wamalize mgogoro ili mwenye haki apewe, tusichotaka kusikia ni uvunjifu wa amani kwa raia sehemu yoyote," amesema Matei.
Viongozi wanaotajwa kukamatwa na Polisi ni pamoja na Askofu wa dayosisi ya Mbeya Magharibi, Judith Kajela, Mchungaji Atupele Mlawa na Mchungaji Lusajo Sanga.