Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amezionya nchi za Magharibi kutopuuza hatari inayoongezeka ya kuzuka mzozo wa nyuklia kuhusu Ukraine. Amesema kimsingi anaiona Jumuiya ya Kujihami ya NATO kama inayotumika katika vita vya wakala na Urusi kwa kupeleka silaha nchini Ukraine. Katika mahojiano yake marefu yaliyorushwa kwenye televisheni, Lavrov pia amesmea msingi wa makubaliano yoyote ya kuumaliza mzozo wa Ukraine unategemea pakubwa na hali ya kijeshi nchini humo. Waziri Lavrov amevitetea vitendo vya Moscow nchini Ukraine na kuilaumu Marekani kwa ukosefu wa mazungumzo. Ameongeza kuwa hatua ya nchi za Magharibi kupeleka Ukraine silaha nzito na za kisasa, ikiwemo makombora ya kuvilipua vifaru, magari ya kijeshi na ndege zisizoruka na rubani ni hatua za uchokozi zinazolenga kurefusha vita hivyo badala ya kuvimaliza.