Ummy Msika (45), mkazi wa kata ya Bomambuzi manispaa ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro amepata madhara mwilini baada ya rafiki yake kudaiwa kumpa maji ya uponyaji ‘upako’.
Msika aliyelazwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa ya Mawenzi amesema wakati akiumwa mguu rafiki yake alimwambia atampa maji hayo ya uponyaji kwa ajili ya kunywa na kupaka.
Ameieleza Mwananchi Digital leo Jumapili kuwa baada ya kunywa maji hayo Aprili mosi, 2022 kutibu tatizo lake la mguu alianza kuumwa na kupoteza hamu ya kula, kuanza kuwashwa sehemu za siri na kwamba kila kukicha tatizo lilikuwa likizidi na hali yake kuwa mbaya na ndugu zake walimchukua na kumpeleka hospitali.
"Aprili mosi nilikuwa siumwi kabisa zaidi ya mguu wangu uliokuwa ukinisumbua, siku hiyo nilikutana na rafiki yangu ambaye kuna kipindi nilikuwa nina shida na maji ya baraka akasema atanipa lakini baadaye tulipotezana.”
"Bahati nzuri nikakutana naye tena akanipa yale maji nikasema tu ngoja ninywe nikapiga nguchu tatu (mafunda matatu) lakini pia akanambia nikisikia sehemu yoyote nawashwa nipake yale maji nikafanya hivyo,” amesema.
Amesema hapo ndipo alipoanza kupoteza ladha ya chakula na kuanza kutoka harahara kwenye maeneo anayowashwa na hata alipopaka maji aliendelea kuwashwa.
Amebainisha kuwa hadi leo Jumapili Aprili 24, 2022 hali yake ni mbaya na ana maumivu makali kutokana na majeraha makubwa aliyonayo hasa sehemu za siri ambazo zina vidonda.
Mwanamke huyo ameviomba vyombo mbalimbali vya uchunguzi kuchunguza maji hayo kujua kama yalikuwa ni maji ya baraka ama la.
Naye mmoja wa madaktari anayemhudumia mwanamke huyo kwa sharti la kutotajwa jina lake amesema wanaendelea kumpatia matibabu kadri ya uwezo wao.
"Haki ya mgonjwa lazima ilindwe na hatuwezi kusema kila kitu ila mgonjwa tunaendelea kumpatia matibabu na tumeshauri ndugu zake waombe mamlaka za kiuchunguzi, maana inadaiwa alikunywa maji ya baraka na yakamletea madhara hayo. Lengo ni maji haya kupimwa sisi hapa tunatibu ila wapo watu wa kuchunguza tukio kama hilo," amesema.
Naye diwani wa Bomambuzi, Juma Raibu aliyefika kumjulia hali mwanamke huyo ameviomba vyombo vya uchunguzi likiwemo Jeshi la Polisi kuchunguza maji hayo kutokana na namna Ummy alivyopata majeraha.
"Nimefika hapa Mawenzi baada ya kupigiwa simu na huyu mwananchi wangu kwa kweli nimeona namna alivyopata majeraha mkubwa na hata vyombo vya uchunguzi tunaviomba kuchunguza hili tukio ili kujua ukweli wa haya maji ambayo alidhani angetumia angeweza kupona," amesema Raibu