WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa
wito kwa Watanzania wenye tabia ya kuwaficha watoto Wenye Ulemavu
kuacha mtindo huo badala yake wahakikishe wanawapa fursa ya kupata
elimu.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Aprili 21, 2022) alipofuturu
na watoto wenye mahitaji maalum wa kituo cha Buigiri, Wilayani Chamwino
ambacho kinamilikiwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central
Tanganyika.
Amesema kuwa ili kuhakikisha watoto hao wanapata
Elimu, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia mahitaji
mbalimbali kwa ajili kujifunza na kufundishia.
Naye, Naibu
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
Mwanaidi Ali Khamisi amesema kuwa tukio hilo ni ishara ya upendo wa
viongozi wakuu wa Serikali kwa kundi la watu wenye mahitaji maalum.
Kwa
upande wake Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central
Tanganyika Dkt. Dickson Chilongani ameshukuru Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa kwa uamuzi wake wa kuamua kula futari na watoto wenye mahitaji
maalum wa kituo cha Buigiri, Wilayani Chamwino
Aidha Askofu Dkt.
Chilongani amemuhakikishia Waziri Mkuu kuwa Kanisa hilo linaendelea
kuiunga mkono Serikali ya awamu ya Sita katika shughuli mbalimbali za
kimaendeleo na kudumisha amani.