Kenya imekataa ombi la Ukraine la kuhutubia bunge la Kenya, serikali ikihofia kuingizwa katika mzozo wa Ukraine na Urusi na kusambaratisha uswahiba wa Nairobi na Moscow.
Serikali Yakataa Ombi la Ukraine la Kuhutubia Bunge la Kenya: "Msitukosanishe"
Taarifa ziliibuka mnamo Jumatatu, Aprili 11, wataalam wa masuala ya kigeni wa serikali ya Kenya wakihoji kuwa tayari wamekuwa wakifanya kila wawezalo kupitia kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN).
Ukraine ambayo imekuwa ikilinda ardhi yake dhidi ya uvamizi wa Urusi iliwalisha ombi hilo mwezi Februari, vikosi vya Urusi vilipoanza mashambulizi.
Kwa mujibu wa gazeti la Nation, ombi hilo halikukubaliwa huku Wizara ya Mambo ya Kigeni ikiamua kucheza kimya licha ya kukumbushwa mara kadhaa na Ukraine.
Gazeti hilo linasema kuwa afisa mmoja mkuu katika wizara hiyo ameliambia kuwa hakuna haja ya kuruhusu hotuba hiyo na kwamba utawala wa Kyiv nafaa kutumia njia za kidiplomasia zilizopo.
Maafisa katika wizara hiyo wameambia the Nation kuwa wamekuwa wakifanya wajibu wao kama wawakilishi wa Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) na lazima wawe makini ili wasionekane kuegemea upande wowote.