Ajali yaua sita Korogwe

Korogwe. Watu sita wamefariki dunia na wengine 19 wamejeruhiwa baada ya basi dogo aina ya Coaster kupinduka katika eneo la kwa Mdulu Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Safia Jongo amesema ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo Jumanne Aprili 12, 2022.

Kamanda Jongo amesema ajali hiyo imetokea baada ya gari hilo lililokuwa linatoka Dar es salaam kwenda Kilimanjaro kuacha njia na kupinduka

"Waliofariki ni wanawake watatu na wanaume watatu ambapo katika hao wanawake mmoja ni mtoto anayekadiriwa kuwa na miaka mitatu na maiti watano wametambuliwa na ndugu zao mmoja bado hajataambuliwa,” amesema.

Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe- Magunga huku majeruhi wakiendelea kupata matibabu hospitalini hapo.

Amebainisha chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi ambapo dereva alishindwa kukata kona na gari kuteleza kisha kupinduka.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Dk Salma Swedi amethibitisha kupokea miili sita na majaruhi 19 na kwamba majeruhi wawili hali zao ni mbaya na wanatarajiwa kupelekwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii