Takriban watu 26 wakiwemo watoto wauawa na watu wenye silaha Nigeria

Watu wenye silaha wameshambulia vijiji vya jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria na kuua takriban watu 26.

Washambuliaji hao waliokuwa kwenye pikipiki walivamia takriban vijiji vinne vya mbali siku ya Jumapili katika eneo la Kanam katika jimbo hilo na kuwapiga risasi watu.

Wengi wa waathiriwa walikuwa watoto. Watu hao wenye silaha pia waliiba ng'ombe na kuchoma nyumba.

Wakazi wanasema takriban miili 20 imepatikana katika kijiji cha Gyambau huku takriban sita ikipatikana katika kijiji cha Kyaram.

Mauaji zaidi yaliripotiwa katika vijiji vya Dungur na Kukawa. watu wengine bado hawajulikani walipo na mamia wamelazimika kuyahama makazi yao.

Mamlaka inasema vikosi zaidi vya usalama vinatumwa katika eneo hilo.

Shambulio la hivi punde linakuja wakati Nigeria ikikabiliana na wimbi la ghasia za magenge yenye silaha ambayo mara kwa mara yanatekeleza mauaji na utekaji nyara ili kujipatia fidia.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii