Watu wasiopungua 35 wamekufa leo na wengine zaidi ya 100 wamejeruhiwa baada ya roketi kukipiga kituo cha treni katika mji wa Kramatorsk kinachotumika kuwaondoa raia wanaokimbia vita mashariki mwa Ukraine. Duru za habari kutoka eneo la mkasa huo zimearifu juu ya hali ya kutisha ikiwemo kutapakaa kwa miili ya watu na dimbwi la damu muda mfupi baada ya kutokea shambulizi hilo. Taarifa juu ya idadi ya vifo na wale waliojeruhiwa imethibitishwa na mkuu wa kampuni ya reli nchini Ukraine, Alexander Kamyshin ambaye pia amesema shambulizi hilo limefanywa kwa kusudi kuhujumu miundombinu ya reli na wakaazi wa mji huo. Ingawa haijafahamika mara moja upande uliohusikana na shambulio hilo, mamlaka nchini Ukraine ziliwataka waakazi wa mashariki kuondoka baada ya kuwepo uwezekano wa kutokea mashambulizi kutoka kwa vikosi vya Urusi.