Nigeria yasema shambulizi la anga limeuwa wanamgambo 70

Jeshi la anga la Nigeria limesema limewauwa zaidi ya wapiganaji 70 wenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo uliko mpaka na taifa jirani la Niger. Msemaji wa kikosi hicho amesema operesheni maalum ilifanywa mnamo Aprili 14 katika kitongoji cha Tumbun Reg baada ya kubainika kile kinachodhaniwa kuwa kambi ya mipango iliyokuwa na idadi kubwa ya wapiganaji wa itikadi kali. Kulingana na afisa huyo wa jeshi operesheni hiyo ilitekelezwa kwa pamoja kwa kutumia ndege za Nigeria na zile za Niger na ilifanikiwa kuwauwa au kuwajeruhi vibaya zaidi ya wanamgambo 70. Eneo hilo la Mto Chad ambalo Nigeria inasema imetekeleza operesheni yake linafahamika kuwa maficho ya wapiganaji wa kundi la itikadi la ISWAP ambao pamoja na makundi mengine wanahusika na vifo vya maelfu ya raia na mamilioni wengine kuyakimbia maakazi yao.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii