Meli ya mafuta yazama pwani ya Tunisia

Meli iliyobeba tani 750 za mafuta ya dizeli ikitokea Misri kwenda kisiwa cha Malta imezama nje kidogo ya pwani ya kusini mashariki mwa Tunisia, lakini maafisa wanasema inawezekana umwagikaji mkubwa wa mafuta huenda utaepukwa. Mabaharia wa meli hiyo ya Xelo walitoa maombi ya msaada na kutafuta hifadhi katika eneo la bahari la Tunisia kutokana na hali mbaya ya hewa, kabla ya meli hiyo kuzama katika Ghuba ya Gabes jana Jumamosi. Waziri wa mazingira wa Tunisia, Leila Chakhaoui, amesema katika mahojiano na televisheni ya taifa kuwa hali imedhibitiwa, huku msemaji wa mahakama mjini Gabes, Mohamed Karray, akiongeza kuwa kuna uvujaji mdogo sana wa mafuta kutoka chombo hicho. Meli hiyo yenye urefu wa mita 58 na upana wa mita 9 ilikuwa inatokea bandari ya Damietta nchini Misri kuelekea kisiwa cha Ulaya cha Malta ilipoomba kuingia katika eneo la bahari la Tunisia.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii