Bunge lanusa matumizi mabaya fedha za Uviko

Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (Usemi) imesema ufuatiliaji umeonyesha kuwa zipo dalili za baadhi ya halmashauri kutotekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia bajeti badala yake kutumia fedha za Uviko.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dennis Londo amesema hayo leo Alhamisi Aprili 14, 2022 wakati akiwasilisha maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2022/2023.

 “Ufuatiliaji wa Kamati umeonesha kuwa zipo dalili kwamba, baadhi ya halmashauri hazikutekeleza miradi iliyopangwa kwenye bajeti zao za ndani, badala yake zimetumia fedha za Uviko kuendeleza miradi hiyo. Kamati imeona sio jambo linalofaa,”amesema.

Amesema uchambuzi unaonesha kwamba, kwa ujumla upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika bajeti ya mwaka 2021/2022 haukuwa kama ulivyotarajiwa.

Amesema hali hiyo, si dalili nzuri kwa utekelezaji bora wa miradi ya maendeleo.

Amesema ni maoni ya Kamati kuwa ubora wa miradi utakuwa na maana iwapo utekelezaji wake utakwenda kama ilivyopangwa.

Aidha, Londo amesema utekelezaji wa miradi unategemea pamoja na mambo mengine, upatikanaji wa fedha iliyoidhinishwa kwa wakati.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii