Viongozi wa Ufaransa na Ujerumani wamekataa kurejelea kauli aliyoitoa rais wa Marekani Joe Biden kwamba Urusi inatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Ukraine na kuonya kwamba kauli kama hizo haziwezi kukomesha vita. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema viongozi wanapaswa kuwa makini na waangalifu juu ya lugha wanayotumia haswa kutaja mauaji ya kimbari katika hali ya sasa kutokana na undugu na ukaribu wa mataifa hayo jirani. Kauli yake imelaaniwa na rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky aliyesema ni ya kuumiza kwa kiongozi kushindwa kutamka wazi mauaji hayo kama ya kimbari. Naye Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alizungumzia uhalifu wa kivita nchini Ukraine lakini alijiepusha kutaja mauaji ya halaiki. Wakati huohuo meli ya kivita ya Urusi katika Bahari Nyeusi imeharibiwa vibaya katika mlipuko wa risasi. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa inafuatilia chanzo cha mlipuko huo lakini wafanyakazi wameondolewa. Awali, gavana wa mji wa Odessa nchini Ukraine alisema kuwa vikosi vya nchi yake vimeipiga meli ya Moskva kwa makombora.