Bibi wa miaka 82, mwanawe wagombea mali

Hilda Maeda (82), mkazi wa Mabogini Wilaya ya Moshi, amemuomba Rais Samia Suluhu na mashirika ya kutetea haki za binadamu kuingilia kati, ili kumzuia mwanawe wa kumzaa asimdhulumu mali anazodai kuchuma na mumewe.

Bibi huyo alitaja mali hizo kuwa ni na shamba walilolipata mwaka 1969 na mumewe ambaye sasa ni marehemu, wakati huo mtoto huyo akiwa na miezi mitatu.

Hata hivyo, mtoto huyo, Richard Maeda alipoulizwa na JEMBE FM jana kuhusiana na madai ya mama yake alikanusha na kueleza alinunua shamba hilo, huku akimtaka mama yake aonyeshe nyaraka kuthibitisha madai yake.

“Mali nilizonazo ni za kwangu, hakuna mahali nimehodhi mali ya familia, wakueleze niliingiaje hapo mwaka 2019 na wakuonyeshe nyaraka zinazoonyesha hilo shamba ni mali ya familia,” alisema Richard.

Akizungumza naJEMBE FM jana, bibi Maeda alisema mjukuu wake mmoja alishamwaga mchanga na mawe katika eneo hilo kwa ajili ya kuanza ujenzi na kudai kwamba Richard ameviuza vyote hivyo.

“Naomba wadau na wanasheria wanisaidie, lakini pia naomba hili limfikie Rais Samia, anisaidie kupata haki yangu. Eneo hilo lirudi mikononi mwangu,” alieleza.

Alisema awali Richard alikuwa akifanya kazi kampuni ya TPC, baada ya kufukuzwa baba yake alimtafutia kazi nyingine na alipoharibu tena na kufukuzwa, ndipo aliporudi nyumbani na kukaa bila kazi.

Baada ya kukaa bila kazi, baba yake alimpeleka mtoto huyo (Ricahrd) na shemeji yake katika shamba hilo na kuwagawia nusu heka na kuwataka watumie eneo hilo kufyatua matofali, ili kupata mtaji na fedha ya kumudu familia zao.

Alisema walifanya kazi na shemeji yake katika shamba hilo na baadaye shemeji huyo aliondoka kwenda mkoani Singida na kumuacha Richard akiendelea na kazi hiyo, lakini baadaye aliwapangisha watu wengine waendelee na kazi hiyo.

Bibi huyo alieleza kuwa mwaka 2020, mumewe, Asri Maenda alilitenga shamba hilo kwa ajili wajukuu wake.

Alieleza wakiwa kwenye maombolezo, alimuona Richard akilima shamba lote na alipoulizwa alidai alipewa na baba yake na hata kanisa na kijiji viliingilia kati jambo hilo bila mafanikio.

Pamoja na jitihada zote hizo, alieleza kuwa Richard aliendelea kung’ang’ania shamba hilo na kwa sasa kuna mtu anajenga nyumba katika shamba hilo.

“Mtu huyo anadai kuwa Richard amekula fedha zake nyingi, ingawa hajafafanua ni kwa namna gani.

“Nilipokwenda pale nilikuta watu wakiendelea na ujenzi, wakaniuliza kama najipenda kweli, sikuwajibu. Nikaambiwa niondoke na Richard alikuwepo akaniambia unasikia ulichoambiwa, ikabidi niondoke nirudi nyumbani,” alieleza.

Kulingana na maelezo ya bibi huyo, baada ya tukio hilo alikwenda ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Moshi na kuagizwa aende Polisi ambako alifungua taarifa ya kutishiwa kuuawa, lakini hakuna hatua stahiki zimechukuliwa hadi sasa.

Mwenyekiti wa zamani wa kijiji hicho, Leonard Mushi alisema anachofahamu na anachokumbuka ni kwamba mtoto huyo na mwenzake walipewa nusu heka na kuambiwa wafyatue matofali, ili apate mtaji na kuendelea na mambo yake.

“Wakati baba yake anampa shamba hilo alimwambia afyatue tofali apate mtaji afanye mambo yake na alimpa nusu heka na hicho ndicho mimi ninachofahamu,” alisema Mushi ambaye wakati Richard akipewa eneo hilo alikuwa kwenye uongozi.

Kwa upande wao, Anaeli Maeda na Eline Maeda ambao ni ndugu wa Richard walwalionyesha kushangazwa na anachokifanya mdogo wao na kueleza kuwa wanachokifahamu ni kwamba shamba hilo ni mali ya familia.

“Tunachofahamu shamba lile ni la mama na baba na Richard alipopata matatizo kazini alipewa yeye na shemeji yake, ili wapate fedha za kujikimu kimaisha,” alisema Eline ambaye ni dada yake Richard.

Baba yao mkubwa, Elifuraha Maeda alieleza kuwa wamejitahidi kuusuluhisha jambo hilo mara kadhaa bila mafanikio na kwamba kila wanapoitisha kikao cha ukoo Richard amekuwa haendi na siku alipokwenda alitaka asiandikwe kwenye mahudhurio kama alifika.

Jumanne Mohamed ambaye ni shemeji yake na Richard waliokabidhiwa eneo la kufyatua matofali ingawa baadae aliondoka Kilimanjaro ila akadai anashangaa kusikia Richard anadai ni shamba lake baada ya baba yake kufariki dunia.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii