Sekta ya filamu nchini Nigeria, imeingia katika majonzi kufuatia kifo cha mwigizaji maarufu Adenike Babajide, anayefahamika kwa jina la kisanii Anike Sinleke.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa Novemba 24, 2026, mwigizaji huyo amefariki dunia baada ya kuugua saratani ya ovari (Ovarian Cancer).
Taarifa za kifo chake zilitolewa Jumapili na mwenzake katika tasnia ya filamu, Bukky Fagbuyi, kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Instagram.
Bukky alieleza kuwa Anike Sinleke alikuwa amepangwa kushiriki katika kipindi chake cha Instagram Live kilichofahamika kama Rubbin Minds With Bukky, lakini kabla ya muda wa mazungumzo hayo kufika, taarifa za kifo chake zilisambaa na kuleta huzuni kubwa.
Anike Sinleke alipata mafunzo ya uigizaji chini ya mkongwe wa filamu Remmy Shitta na baadaye kushiriki katika filamu mbalimbali akifanya kazi pamoja na mtengenezaji wa filamu Deji Adenuga.
Mbali na kazi ya uigizaji, marehemu pia aliingia katika utayarishaji wa filamu, akitoa mchango wake katika kukuza tasnia ya filamu za Kiyoruba nchini Nigeria.
Hata hivyo, baadaye alijiondoa kwa muda katika shughuli za filamu ili kuendelea na masomo yake ya Stashahada ya Juu (HND).
Kifo chake kimeacha simanzi miongoni mwa waigizaji wenzake, mashabiki na wadau wa tasnia ya burudani, huku salamu za rambirambi zikiendelea kutolewa.